2 Kings 6

Shoka Laelea

1 aWana wa manabii wakamwambia Al-Yasa, “Tazama, mahali hapa tunapokutana nawe ni padogo sana kwetu. 2Twendeni Yordani, mahali ambapo kila mmoja wetu anaweza kupata nguzo moja, nasi tujenge huko mahali petu pa kuishi.”

Naye akawaambia, “Nendeni.”

3Kisha mmoja wao akasema, “Je, tafadhali, huwezi kufuatana na watumishi wako?”

Al-Yasa akajibu, “Nitakuja.”
4Naye akaenda pamoja nao.

Basi wakaenda Yordani, nao wakaanza kukata miti.
5Mmoja wao alipokuwa anakata mti, shoka lilitumbukia kwenye maji. Akalia, “Ee bwana wangu, shoka lilikuwa la kuazima!”

6 bMtu wa Mungu akauliza, “Je, liliangukia wapi?” Alipomwonyesha mahali penyewe, Al-Yasa akakata kijiti na kukitupa mahali pale, nalo shoka likaelea. 7Akasema, “Lichukue.” Kisha yule mtu akanyoosha mkono wake, akalichukua.

Al-Yasa Awanasa Waaramu Waliopofushwa

8Wakati huo mfalme wa Aramu alikuwa akipigana vita na Israeli. Baada ya kukubaliana na maafisa wake, akasema, “Nitapiga kambi yangu mahali fulani na fulani.”

9 cMtu wa Mungu akatuma ujumbe kwa mfalme wa Israeli: “Jihadhari usije ukapita mahali pale, kwa sababu Waaramu wanashuka huko.” 10Kwa hiyo mfalme wa Israeli akatuma neno la tahadhari mahali pale alikokuwa ameelekezwa na mtu wa Mungu. Mara kwa mara Al-Yasa alimwonya mfalme kwamba watu wawe macho kwenye maeneo kama hayo.

11Hili lilimfadhaisha sana mfalme wa Aramu. Akawaita maafisa wake, akawauliza, “Je, hamtaniambia ni nani miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?”

12Mmoja wa maafisa wake akasema, “Mfalme bwana wangu, hakuna hata mmoja wetu. Lakini Al-Yasa, yule nabii aliye Israeli, humwambia mfalme wa Israeli hata yale maneno unayozungumza katika chumba chako cha kulala.”

13 dMfalme akaagiza akisema, “Nendeni, mkatafute aliko, ili niweze kutuma watu kumkamata.” Taarifa ikarudi kwamba, “Yuko Dothani.” 14Ndipo akatuma farasi na magari ya vita na jeshi lenye nguvu huko. Walikwenda usiku na kuuzunguka mji.

15Kesho yake asubuhi na mapema, mtumishi wa mtu wa Mungu alipoamka na kutoka nje, jeshi, pamoja na farasi na magari ya vita, likawa limeuzunguka mji. Mtumishi wake akasema, “Ole wetu, bwana wangu! Tutafanya nini?”

16 eNabii akajibu, “Usiogope. Wale walio pamoja nasi ni wengi zaidi kuliko wale walio pamoja nao.”

17Kisha Al-Yasa akaomba, “Ee Bwana, mfumbue macho huyu mtumishi ili apate kuona.” Ndipo Bwana akayafumbua macho ya yule mtumishi, naye akatazama na kuona vilima vimejaa farasi na magari ya moto, yamemzunguka Al-Yasa pande zote.

18 fWakati adui waliposhuka kumwelekea, Al-Yasa akamwomba Bwana: “Wapige watu hawa kwa upofu.” Basi Mungu akawapiga kwa upofu, kama Al-Yasa alivyoomba.

19Al-Yasa akawaambia, “Hii sio njia yenyewe, na huu sio huo mji. Nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa huyo mtu mnayemtafuta.” Naye akawapeleka Samaria.

20Baada ya kuingia mjini, Al-Yasa akasema, “Bwana, yafungue macho ya watu hawa ili wapate kuona.” Ndipo Bwana akayafungua macho yao, na walipotazama, kumbe hapo ndipo walipojikuta, ndani ya Samaria.

21 gWakati mfalme wa Israeli alipowaona, akamuuliza Al-Yasa, “Je, baba yangu, niwaue?”

22 hNaye akajibu, “Usiwaue. Je, utawaua watu uliowateka kwa upanga wako mwenyewe na upinde wako? Wape chakula na maji ili wapate kula na kunywa, na kisha wamrudie bwana wao.” 23 iBasi akawaandalia karamu kubwa, na baada ya kula na kunywa, akawaaga nao wakarudi kwa bwana wao. Hivyo, vikosi kutoka Aramu vikakoma kuvamia nchi ya Israeli.

Njaa Katika Samaria Iliyozingirwa

24 jBaada ya kitambo kidogo, Ben-Hadadi mfalme wa Aramu akaandaa jeshi lake lote akapanda kwenda kuihusuru Samaria. 25 kKukawa na njaa kuu katika mji. Samaria ilizingirwa kwa muda mrefu, kiasi kwamba kichwa cha punda kiliuzwa kwa shekeli themanini
Shekeli 80 za fedha ni sawa na kilo moja.
za fedha, na robo ya kibaba
Robo ya kibaba ni sawa na lita 0.3.
cha mavi ya njiwa kiliuzwa kwa shekeli tano
Shekeli tano za fedha ni sawa na gramu 55.
za fedha.

26Wakati mfalme wa Israeli alipokuwa anapita juu ya ukuta, mwanamke mmoja akamlilia, “Bwana wangu mfalme, nisaidie!”

27Mfalme akajibu, “Ikiwa Bwana hakusaidii, nitakutolea wapi msaada? Je, ni kutoka kwenye sakafu ya kupuria? Au kwenye shinikizo la divai?” 28Kisha akamuuliza, “Kwani kuna nini?”

Yule mwanamke akamjibu, “Huyu mwanamke aliniambia, ‘Mtoe mwanao ili tupate kumla leo, na kesho tutamla mwanangu.’
29 oBasi tukampika mwanangu na kumla. Siku iliyofuata nikamwambia, ‘Mtoe mwanao ili tupate kumla.’ Lakini akawa amemficha.”

30 pWakati mfalme aliposikia maneno ya yule mwanamke, alirarua mavazi yake. Naye alipoendelea kutembea ukutani, watu wakamtazama, na ndani ya mavazi yake alikuwa amevaa nguo ya gunia mwilini mwake. 31Akasema, “Mungu na anitendee hivyo na kuzidi, ikiwa kichwa cha Al-Yasa mwana wa Shafati kitabaki juu ya mabega yake leo!”

32 qWakati huu, Al-Yasa alikuwa ameketi ndani ya nyumba yake, akiwa pamoja na wazee. Mfalme akatuma mjumbe kumtangulia, lakini kabla hajafika, Al-Yasa akawaambia wale wazee, “Hammwoni huyu muuaji jinsi anavyotuma mtu kukata kichwa changu? Tazama, wakati mjumbe huyo atakapofika, fungeni mlango na mzuieni asiingie. Je, vishindo vya nyayo za bwana wake haviko nyuma yake?”

33 rAlipokuwa angali bado anazungumza nao, mjumbe akamfikia. Naye mfalme akasema, “Maafa haya yanatoka kwa Bwana. Kwa nini niendelee kumngoja Bwana zaidi?”
Copyright information for SwhKC